HUU HAPA UCHAMBUZI WA KLABU YA YANGA YENYE MAJERUHI ZAIDI YA 10 HUKU IKIENDELEA KUFANYA MAAJABU

Mkubwa ni mkubwa tu. Hakuna ubishi sasa, Yanga imezidi kuthibitisha kwamba ndio timu kubwa zaidi nchini. Inafanya kile ambacho watu hawajakitazamia.

Ikiwa na majeruhi zaidi ya 10, Yanga imeshinda mechi za tatu za ligi mfululizo jana wameichapa Njombe Mji mabao 4-0, pia ilivunja mwiko mjini Iringa na kuifunga Lipuli mabao 2-0 na awali wakaiduwaza Azam nyumbani kwake kwa kuifunga mabao 2-1.

Inafurahisha sana.
Imefikia hatua Yanga imeishiwa mabeki wa kati na kwenye mechi ya iliyopita, ilimchezesha Said Juma 'Makapu' kwenye nafasi hiyo lakini haikuruhusu bao. Huwa inatokea mara chache sana.

Mabeki wa kati, Nadir Haroub 'Cannavaro', Andrew Vincent 'Dante' na Abdallah Shaibu wote ni wagonjwa. Yule beki wao Mkongomani, Fiston Kayembe bado hajapata hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Nani angecheza nafasi hiyo? Ilibidi awe Makapu.

Upande wa pili, kwenye benchi Yanga ilikuwa na kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili ambaye alilazimika kuanza dhidi ya Njombe mji ikiwa ni siku tatu tangu alipoingia dakika ya 15 baada ya kipa namba moja, Youthe Rostand kuumia. Nani aliwahi kuwaza kwamba Kabwili anaweza kudaka mechi ya Ligi Kuu bila kuruhusu bao? Imetokea pale Iringa na Dar es Salaam.

Kipa namba mbili, Beno Kakolanya naye ni mgonjwa. Yanga inalazimika kutumia wachezaji waliopo. Wachezaji hawashindanii nafasi tena kwani wengi ni majeruhi.

Ushindi huo wa Yanga unatoa taswira mbili. Kwanza, wadau wa soka nchini wasiibeze kwani inaweza kupunguza wigo wa pointi baina yake na Simba muda wowote. Pili, wachezaji wa Yanga wanajitambua na wanafahamu wapo kwenye hali gani. Wanacheza kwa ajili ya timu.

Pamoja na yote, Pius Buswita na Obrey Chirwa wamezidi kuwa watamu. Kazi waliyoifanya kwenye mchezo huo, inazidi kuwapandisha chati. Buswita amezidi kuwa mbunifu. Wakati Chirwa amefikisha mabao 10 na kumtishia Emmanuel Okwi wa Simba mwenye mabao 12.

No comments: