Breaking News: HABARI MPYA ZILIZOTUFIKIA HIVI PUNDE KUTOKA KLABU YA SIMBA....KOCHA AFUNGUKA ASUBUHI ASUBUHI....
Klabu ya Simba imevuna mabao 15 katika mechi tano zilizopita huku ikiwa haijaruhusu bao kwenye michezo hiyo ya hivi karibu, hivyo kuifanya hadi sasa kucheka na nyavu mara 38 kufuatia kushuka dimbani mara 16 tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
Matokeo hayo yameifanya Simba kuwa timu yenye kasi zaidi ya kufunga msimu huu huku pia ikiwa na ukuta mgumu zaidi baada ya kuruhusu mabao sita pekee msimu huu.
Kocha msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma, amedokeza siri ya mafanikio hayo wanayoendelea kuyapata kuwa yanatokana na mbinu zao za uchezaji zinazowafanya wapinzani wao kushindwa kuendana na kasi yao.
Djuma alisema kucheza zaidi soka mbali na lango lao uwanjani ni moja ya siri ya ushindi wao wa mfululizo na kutoruhusu mabao.
"Kucheza mbali na lango letu kwa maana ya kucheza karibu na eneo la adui linatupa nafasi kubwa yakujilinda na kupata mabao," alisema Djuma.
"Ni kwamba kucheza zaidi kwenye lango la adui kunamuongezea presha mpinzani wetu, na ikitokea akafanya makosa kidogo tunamuadhibu, lakini pia tumekuwa tukibadilika badilika katika kila mchezo," aliongeza kusema Djuma.
Alisema pamoja na ushindi walioupata juzi dhidi ya Ruvu Shooting, bado kazi hawajamaliza na wataendelea kupambana kwa uwezo wa juu mpaka mchezo wao wa mwisho msimu huu.
"Ila bado yapo makosa mdogo madogo ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi, soka la sasa ni la mbinu zaidi, nashukuru wachezaji wamekuwa wepesi kushika na kufuata maelekezo," aliongeza kusema.
"Hatutafanya makosa tena kwa Azam kuelekea kwenye mchezo wa kesho (leo) dhidi yao," alisema Djuma na kuongeza kuwa ushindi ndio jambo pekee wanalolitaka na hawatafanya makosa waliyoyafanya kwenye mchezo wa kwanza ambao walishindwa kufungana.
"Azam ni timu nzuri, kama tunavyojiandaa kwenye michezo mingine, ndivyo tunavyojiandaa dhidi ya Azam, kikubwa ni lazima tubaki kwenye mfumo wetu na mbinu zetu," alisema Djuma.
Endapo Simba itafanikiwa kupata ushindi dhidi ya Azam, itawafanya kuwaacha wapinzani wao hao kwa pointi nane na kuzidi kukoleza kasi kuelekea kutwaa ubingwa msimu huu.
No comments: