HII NI HATARI: MAPYA YAIBUKA KUHUSU OBREY CHIRWA.
WIKI chache zilizopita, Mzambia Obrey Chirwa, alikuwa gumzo si kwa kitendo chake cha kukomalia kwao kujishughulisha na kilimo cha mahindi na matikiti, bali ilikuwa ni kwa kukosa penalti katika nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Kitendo chake cha kutupia mtandaoni picha za shambani na kisha kuja kukosa penalti iliyoifungisha virago Yanga, kiliwafanya watani zao Simba kupata msemo na hata baadhi ya mashabiki wa Yanga walianza kumgeuka, lakini ghafla jamaa amekuwa mtamu kiasi cha kusisimua.
Straika huyo juzi Jumanne alipiga Hat Trick na kumfanya afikishe mabao kumi wakati Yanga ikiizamisha Njombe Mji 4-0, lakini kama hujui katika mabao hayo straika huyo ametengeneza rekodi nyingine msimu huu.
Chirwa anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga Hat Trick mbili msimu huu na kumzidi Emmanuel Okwi, aliyekuwa na Hat Trick moja ya haraka katika VPL, huku akiongoza orodha ya ufungaji kwa kutupia mabao 12 mpaka sasa.
Hakuna aliyefikia rekodi ya kufunga Hat Trick ya haraka na pia kutupia mabao manne katika mechi moja msimu huu, lakini Chirwa amefunika kweli kweli na kama wapinzani wake hawatajipanga, jamaa ataendelea kuwanyoosha.
Katika ushindi huo wa 4-0, Chirwa pia alimpiku John Bocco kwa bao moja baada ya kuwa na mabao 10 dhidu ya tisa wa Bocco (kabla ya mechi ya jana ya Simba), huku akipitwa mabao mawili dhidi ya Okwi (pia kabla ya mechi hiyo ya jana ya Simba na Azam).
Hata hivyo Chirwa alikosekana uwanjani katika michezo kadhaa kutokana na kwenda kwao Zambia, kutokana na matatizo yake ya kifamilia, lakini hata aliporudi alikutana na kitanzi cha kufungiwa na Kamati ya Saa 72 kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Chirwa ameonyesha kuwa kadiri ligi itakavyosonga mbele ndivyo atakavyowanyosha mabeki wa timu pinzani kwani, jamaa ni hatari akiwa ndani ya 18.
BUSWITA, AJIBU
Kama hujui ni kwamba katika Hat Trick zote alizofunga Chirwa, amepata msaada mkubwa kutoka kwa Ibrahim Ajibu na kiungo Pius Buswita ambao wamekuwa wakimtengenezea mabao kwa ushirikiano mkubwa.
Katika Hat Trick ya kwanza dhidi ya Mbeya City, Buswita alimtengenezea bao moja na juzi alifanya hivyo tena wakati akifunga bao la kwanza, japo naye (Chirwa) pia amekuwa akitengeneza mabao kwa nyota hao.
Buswita amefunga mabao matatu mpaka sasa kama ilivyo kwa Emmanuel Martins, huku Ajibu akifunga matano, japo amekosekana katika mechi za karibuni kutokana na kuwa majeruhi.
Mastraika hao wanne kwa ujumla wao wamepachika wavuni mabao 21 kati ya 26 yaliyowekwa kimiani na Yanga katika mechi zao 17 walizocheza kwenye ligi ya msimu huu mpaka sasa.
No comments: